BILIONI 840 Kutumika Ujenzi wa Miundombinu Iliyoathiriwa na El-nino
JIUNGE NASI TELEGRAM BOFYA HAPA WHATSAPP BOFYA HAPA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali tayari imeelekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 840 (Dola za Marekani Milioni 325) katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na makalvati yaliyoharibiwa na mvua kubwa za El-Nino na Kimbunga Hidaya ambapo maandalizi ya utekelezaji huo yanaendelea.
Ameeleza kuwa mvua za El-Nino zilizonyesha katika kipindi cha mwezi Septemba 2023 hadi Aprili 2024 na kuathiri mawasiliano ya barabara na madaraja, Serikali ilitoa kiasi cha Shilingi Bilioni 72.1 kufanya matengenezo ya dharura katika maeneo yaliyokatika mawasiliano.
Bashungwa ameeleza hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jana Agosti 22, 2024 wakati akiwasilisha taaarifa ya mkakati wa Serikali kuhusu Ukarabati wa Miundombinu ya Barabara iliyoharibiwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya.
“Wizara imeona umuhimu wa kuanza ujenzi wa madaraja na makalvati kwa kuwa mvua inaponyesha pindi kunapokuwa na barabara mawasiliano yanaendelea kuwepo hata kama ni kwa shida lakini daraja ama kalvati linapovunjika linasababisha mawasiliano kukosekana kabisa”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa miundombinu yote iliyoathiriwa inafanyiwa matengenezo ili irudi katika hali yake ya awali ambapo tathimini ilionesha kiasi cha Shilingi Trilioni 1.07 kinahitajika kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu yote iliyoathiriwa.
Aidha, Bashungwa ameielekeza Wakala ya Barabara (TANROADS), kuhakikisha inafanya mapitio mapya ya barabara zilizofanyiwa usanifu miaka ya nyuma ili kuweza kutekeleza ujenzi na matengenezo kulingana na uhalisia, Mabadiliko ya Mazingira, Ongezeko la watu na ukuaji wa Miji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb), ameishauri Wizara ya Ujenzi kushirikisha Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yaliyolengwa ili utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa ufanyike kwa tija na mahitaji halisi ya maeneo husika.
Kakoso ameitaka Wizara ya Ujenzi kuusimamia kikamilifu Wakala wa Barabara (TANROADS) na Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kuhusu upatikanaji wa vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo mpana wa kupata fedha kwa ajili ya mipango ya baadae ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja.
PATA NYIMBO ZOTE MPYA BONYEZA HAPA
MATANGAZO YA BIASHARA WASILIANA NASI KUPITIA nijuzehabariblog@gmail.com
Tags: BILIONI 840 Kutumika Ujenzi wa Miundombinu Iliyoathiriwa na El-nino