HESBL Maswali Yanayoulizwa Mara Kwa Mara 2024/2025
JIUNGE NASI TELEGRAM BOFYA HAPA WHATSAPP BOFYA HAPA
HESBL Maswali Yanayoulizwa Mara Kwa Mara 2024/2025, Maswali 25 pamoja na majibu
yake yameandaliwa kumwezesha mwombaji,
mzazi, mlezi au mtoa huduma kwa mwanafunzi
kuelewa kwa lugha rahisi utaratibu, sifa na vigezo vitakavyotumika katika upangaji mikopo kwa mwaka 2024/2025.
Ingawa Maswali na Majibu haya yamebeba
maudhui ya miongozo iliyotolewa, waombaji
mikopo na ruzuku kwa ngazi ya stashahada
(Diploma), shahada ya awali (Bachelor Degree),
stashahada ya uzamili katika mafunzo ya sheria kwa vitendo (Post Graduate Diploma in Legal Practice), Samia Skolashipu na Shahada za Umahiri na Uzamivu (Master and PhD) wanashauriwa kusoma miongozo mahsusi ambayo ina maelezo ya kina kuhusu maeneo yao.
Miongozo hii inapatikana katika tovuti
ya HESLB www.heslb.go.tz.
MASWALI YA MARA KWA MARA KUHUSU UOMBAJI MIKOPO HESBL
Swali: Je, ni wakati gani naweza kuomba mkopo wa elimu ya juu?
Jibu: Maombi ya mkopo hufanyika mara moja kwa kila mwaka wa masomo. Kwa mwaka2024/2025, maombi yatapokelewa kwa
njia ya mtandao kuanzia June 01 hadi September 14, 2024.
Swali: Zipi ni sifa kuu za kupata mkopo wa elimu ya juu?
Jibu: Mwombaji wa mkopo anapaswa
kuwa na sifa kuu zifuatazo:
- Awe mtanzania;
- Awe ameomba mkopo kwa njia ya mtandao kama inavyoelekezwa;
- Awe amepata udahili (admission) na uliothibitishwa kwenye chuo kinachotambuliwa;
- Asiwe na chanzo kingine cha kugharimia masomo yake ya elimu ya juu kama ufadhili mwingine, ZHELB n.k;
- Aidha, mwombaji anashauriwa kusoma maelezo ya kina kuhusu sifa na vigezo katika ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo
kwa 2024/2025’ unaopatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz)
Swali: Ni nyaraka gani muhimu zinatakiwa wakati wa kuomba mkopo?
Jibu: Nyaraka muhimu zinazotakiwa ni kama
ifuatavyo:
- Namba ya Uhakiki (Verication Code) ya Cheti cha kuzaliwa cha mwombaji iliyotolewa na RITA au nakala ya cheti kilichohakikiwa na ZCSRA
- Nakala ya cheti cha Stashahada (Diploma) kwa
- waombaji waliohitimu stashahada wanaojiunga na shahada ya awali (Bachelor Degree);
- Namba ya Uhakiki (Verication Code) ya Cheti cha kifo
- kutoka RITA ikiwa mwombaji amepoteza mzazi/wazazi au nakala ya cheti kilichothibitishwa na ZCSRA;
- Nakala ya Kitambulisho cha mdhamini (NIDA, Kadi ya mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Pasi ya Kusafiria au kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi). Mdhamini anaweza kutumia kimoja kati ya vitambulisho hivyo;
- Fomu ya ufadhili iliyojazwa kikamilifu na kusainiwa na mdhamini ikiwa mwombaji alifadhiliwa katika masomo yake sekondari au stashahada. Fomu hii inapatikana kwenye mfumo wakati wa kuomba mkopo;
- Kwa wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu, fomu maalumu iliyojazwa kikamilifu na kuthibitishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya au Mkoa. Fomu hii inapatikana kwenye mfumo wakati wa kuomba mkopo;
- Picha ndogo (passport size) ya mwombaji wa mkopo na ya mdhamini wake
(mdhamini anaweza kuwa mzazi au mlezi).
Swali: Je, ni wapi nitahakiki cheti za kuzaliwa au cheti cha kifo cha mzazi?
Jibu: Vyeti vya kuzaliwa na vya vifo vya wazazi
lazima vihakikiwe na Wakala wa Usajili, Ufilisi
na Udhamini (RITA) au ZCSRA (kwa Zanzibar)
kabla havijapakiwa (uploaded) kwenye
mfumo wa maombi ya mkopo wa HESLB.
Mwombaji mkopo anashauriwa kufuata maelekezo ya taasisi hizi ili kufanya uhakiki wa vyeti.
Swali: Upangaji wa mikopo kwa wanafunzi walioomba na kufanikiwa huzingatia uhitaji upi?
Jibu: Uchambuzi wa kina wa taarifa za mwombaji hufanyika kwa
kuzingatia uhitaji wa mwombaji mkopo. Uhitaji huu hupimwa na king’amua uwezo (Means Testing Tool). King’amua uwezo hutumia taarifa ambazo mwombaji mkopo amejaza na kuthibitishwa na HESLB.
Swali: Je, yatima na wenye ulemavu wanapewa kipaumbele katika uombaji mikopo?
Jibu: Pamoja na sifa kuu zilizotajwa katika jibu Na. 2, upangaji mikopo pia hutoa kipaumbele kwa makundi maalumu kama waombaji yatima, wenye ulemavu au wenye wazazi wenye
ulemavu, na wanafunzi waliofadhiliwa katika masomo ya sekondari au stashahada kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za elimu.
Waombaji mikopo kutoka makundi yaliyotajwa wanapaswa kusoma ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo wa mwaka 2024/2025’ unaoelekeza mambo muhimu ya kuzingatia na nyaraka
zinazotakiwa. Mwongozo huo unapatikana katika tovuti www.heslb.go.tz
Swali: Ninapaswa kufanya nini ili niweze kuanza kuomba mkopo kwa njia ya mtandao (OLAMS)?
Jibu: Soma mwongozo unaotolewa na HESLB ambao unapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz), kisha, fungua
mtandao wa maombi olas.heslb.go.tz ili ujisajili kwa kutumia namba yako ya mtihani wa kidato cha nne na mwaka uliofanya mtihani huo wa kidato cha nne.
MUHIMU: Hakikisha namba unayotumia kuomba mkopo iwe ndiyo unayotumia kuomba udahili (admission) chuoni.
Swali: Baada ya kujisajili kwenye mfumo (OLAMS), napaswa kufanya nini?
Jibu: Baada ya kujisajili kwenye mfumo, mwombaji utapata namba ya kumbukumbu (Control Number) kwenye ‘screen’ ambayo itakuwezesha kufanya malipo ya ada ya maombi ya TZS 30,000/= kwa njia ya benki au simu kwa waombaji wa mikopo
kwa ngazi ya stashahada (Diploma) na shahada ya awali (Bachelor Degree).
MUHIMU: Lipa mara moja tu kiasi kamili cha fedha kilichoainishwa na endelea na maombi kwa kufuata maelekezo.
Swali: Je, Mwombaji anaweza kutumia simu ya mkononi kufanya maombi ya mkopo?
Jibu: Haishauriwi kutumia simu ya mkononi kufanya maombi ya mkopo. Ushauri huu unatokana na uzoefu wa uambatishwaji
wa nyaraka zisizofaa au zenye uhafu kama picha n.k. Ni vema mwombaji akatumia ‘computer’ kwa uhakika wa zaidi.
Swali: Je, mwanafunzi anaweza kupata usaidizi wa kuomba mkopo kwenye ‘Internet Café’?
Jibu: Ndiyo. Hata hivyo, mwombaji ana wajibu muhimu wa kuhakikisha taarifa zake zimejazwa kwa usahihi na ukamilifu.
Ni wajibu wa mwombaji mkopo kuhakikisha viambatisho vyote (vyeti na nyaraka nyingine) vimewekwa/vimepakiwa kwenye fomu yake mtandaoni ili kuepuka maombi yake kutokamilika ipasavyo.
Swali: Kuna uhusiano gani kati ya TCU na HESLB?
Jibu: Zote ni Taasisi za Serikali zinazohudumia wanafunzi wa elimu ya juu.
Tume yaVvyuo Vikuu (TCU) inasimamia udahili (admission) na HESLB inatoa mikopo kwa wanafunzi waliopata udahili katika chuo kinachotambuliwa na Serikali kupitia TCU.
Aidha kwa wanafunzi wanaopata mikopo kwa ngazi ya Stashahada, udahili wao utathibitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Swali: Je, kuna umuhimu wa kuwa na Akaunti ya Benki au Namba ya NIDA wakati wa kuomba mkopo?
Jibu: Ndiyo. Mwombaji mkopo anashauriwa na kusisitizwa kuwa na Akaunti ya Benki yenye majina yake ili kurahisisha malipo
akika chuoni.
Mwombaji anaweza kufungua akaunti katika benki yoyote aipendayo.
Aidha, mwombaji mkopo ahakikishe majina yake yanayotumika katika akaunti ya benki yanafanana na majina yaliyomo kwenye cheti chake cha kidato cha nne.
Kuhusu namba inayotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mwombaji anashauriwa kuiweka (kama anayo). Kama hana, anaweza kuendelea na maombi bila namba hiyo.
Swali: Iwapo niliwahi kupata mkopo miaka iliyopita na nikaacha, kushindwa au kufukuzwa chuo, nitaweza kupata mkopo mwingine?
Jibu: Lengo la mkopo wa elimu ya juu ni kumwezesha mwanafunzi kusoma na kumaliza masomo yake kwa wakati. Hivyo, iwapo
uliwahi kuwa mnufaika wa mkopo wa fedha za Serikali, na hukumaliza masomo, utapaswa kwanza kurejesha mkopo wote wa awali au angalau asilimia 25 ya deni lako kabla ya kukiriwa kupata mkopo mwingine kwa kuzingatia vigezo vya mwaka husika.
Swali: Iwapo nina wazazi wasio na uwezo kiuchumi, niwasilishe uthibitisho gani ili kupata mkopo?
Jibu: Mwombaji ambaye ana mahitaji maalumu, ni lazima mahitaji na hali yake ithibitishwe na mamlaka husika kama Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) au taasisi za aina hiyo zinazotambulika na zinazoweza kuthibitisha.
Swali: Iwapo nilikosa mkopo mwaka jana, nikalazimika kuahirisha masomo, natakiwa kuomba tena mkopo mwaka huu?
Jibu: Unaruhusiwa kuomba upya mkopo mwaka huu. Maombi yako yatapimwa kwa kuzingatia mwongozo na vigezo vya mwaka
husika wa masomo. Unashauriwa usome mwongozo wa mwaka 2024/2025 kwa makini na kuuzingatia.
Aidha, kama unasoma mwaka wa pili au wa tatu na kuendelea na una uhitaji wa mkopo, unaruhusiwa kuomba kwa kuzingatia
vigezo vya mwaka 2024/2025.
Swali: Fomu za maombi ya Mikopo zinawasilishwaje HESLB?
Jibu: Baada ya kukamilisha kujaza fomu ya maombi, kuzipakia (upload) na kuzituma mtandaoni, mwombaji a-print fomu iliyokamilika na kuitunza kwa ajili ya matumizi binafsi au endapo itatokea HESLB kuhitaji fomu hizo.
MUHIMU: Kumbuka, kuanzia mwaka 2023/2024 mwombaji hapaswi kutuma fomu HESLB kwa njia ya posta.
Swali: Mwombaji atajuaje iwapo amepata mkopo?
Jibu: Baada ya HESLB kupokea, kuhakiki na kuchambua maombi ya mikopo, taarifa kwa watakaopangiwa mikopo itatangazwa
kupitia vyombo vya habari, kwenye tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na vyuoni.
MUHIMU: Kila mwombaji mkopo atapata taarifa (status) ya ombi lake kupitia akaunti ya SIPA (Student’s Individual Permanent Account) aliyotumia kuombea mkopo.
Swali: Je, mwombaji anawezaje kufuatilia taarifa za maombi yake?
Jibu: Waombaji mkopo na wanafunzi wanufaika wa mkopo waliopo vyuoni wanaweza kufuatilia mwenendo na taarifa zao kupitia akaunti zao za SIPA.
SIPA ni akaunti ambayo mwombaji ametumia kuomba mkopo na ataendelea kuitumia kupata taarifa mbalimbali hata akiwa chuoni.
Swali: Je, wanafunzi waliopo katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) watapata nafasi ya kuomba mkopo?
Jibu: Wanafunzi waliopo katika mafunzo ya JKT watapata fursa ya kuomba mkopo wa elimu ya juu kwa kuwa dirisha la kuomba
mkopo kwa njia ya mtandao litakuwa wazi kwa siku 90 kuanzia Juni 01 hadi September 14, 2024.
Waombaji mkopo wanahimizwa
kuzingatia muda uliotolewa wa kujaza fomu za maombi ya mkopo.
Swali: Mkopo unatolewa kugharimia maeneo yapi (Loan Items)?
Jibu: Yapo maeneo sita va mikopo. Mwombaji mkopo aliyekidhi vigezo na sifa, anaweza kupangiwa mkopo kugharimia maeneo yote au baadhi kutokana na uhitaji wake. Maeneo
ambayo mwombaji anaweza kupangiwa mkopo ni:
- Chakula na malazi;
- Ada ya mafunzo;
- Vitabu na viandikwa;
- Mahitaji maalumu ya kitivo;
- Utafiti; na
- Mafunzo kwa vitendo
Swali: Je, umri ni kigezo cha kupangiwa mkopo?
Jibu: Umri ni mojawapo ya kigezo cha kupangiwa mkopo kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma masomo ya ngazi ya stashahada (Diploma) na shahada ya awali (Bachelor Degree) ambao unapaswa usizidi miaka 35 na pia muda wa masomo toka mwombaji amehitimu ngazi iliyotangulia usizidi
miaka mitano (2020 – 2024) Maelezo ya kina yamo kwenye miongozo ya kuomba mkopo kwa mwaka 2024/2025 inayopatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo
(www.heslb.go.tz).
Swali: Je, mikopo inatolewa kwa vyuo binafsi?
Jibu: Mikopo inatolewa kwa wanafunzi wahitaji wenye sifa waliodahiliwa katika vyuo vyote vya umma na vya binafsi vinavyotambuliwa na Serikali kupitia TCU na NACTVET kwa
kuzingatia sifa zilizoainishwa katika jibu la Swali Na. 2.
Swali: Je, mikopo inatolewa kwa kuzingatia ufaulu?
Jibu: Kwa mwaka wa kwanza mikopo inatolewa kwa wanafunzi wahitaji wenye sifa baada ya kupata udahili katika vyuo
vinavyotambuliwa na Serikali. Kuanzia mwaka wa pili na kuendelea, mwanafunzi mnufaika atapangiwa mkopo baada ya kuwa amefaulu mitihani yake ya chuo ya mwaka uliotangulia kumwezesha kuingia mwaka unaofuata.
Swali: Je, HESLB inatoa mikopo kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma
masomo ya ngazi ya Stashahada?
Jibu: Kuanzia mwaka wa masomo wa 2023/2024, Serikali imeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaoenda kusoma stashahada
maalumu za Sayansi ambazo zina uhitaji zaidi wa wataalamu.
Mwongozo kuhusu programu hizo na utaratibu wa kuomba kwa mwaka 2024/2025 unapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya
Mikopo (www.heslb.go.tz).
Swali: Je, nifanye nini ili niweze kufadhiliwa gharama za masomo chuoni kupitia “Samia Scholarship”?
Jibu: “Samia Scholarship” ni maalumu kwa wanafunzi wa shahada ya awali (Bachelor Degree) waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita (NECTA) mwaka 2024 katika
Tahasusi za Sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN). Inagharimia kwa asilimia mia moja (100%) masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi hao ambao wamepata udahili katika
fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba. Ufadhili huu utatolewa kwa wahitimu wa kidato cha sita mwaka wenye sifa zifuatazo:
- Awe Mtanzania;
- Awe na ufaulu wa juu kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha sita katika tahasusi za sayansi;
- Awe amepata udahili katika Chuo cha Elimu ya Juu hapa nchini kinachotambuliwa na Serikali katika programu za
Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati au Tiba; - Awe ameomba ufadhili kwa usahihi kwa njia itakayoelekezwa.
Orodha ya majina ya wanafunzi watakaopata ufadhili wa Samia Scholarship itapatikana kupitia tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (www.moe.go.tz) na ya Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (www.heslb.go.tz) baada ya matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka husika kutangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).