MAKUNDI ya CECAFA Kagame Cup 2024
JIUNGE NASI TELEGRAM BOFYA HAPA WHATSAPP BOFYA HAPA
MAKUNDI ya CECAFA Kagame Cup 2024
MAKUNDI ya CECAFA Kagame Cup 2024, Droo ya Michuano ya klabu Bingwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Cecafa Kagame Cup 2024 imekamilika na haya ni Makundi kama yalivyopangwa.
Klabu za Coastal Union ya Tanga na JKU kutoka Zanzibar zimepangwa Kundi A katika Mashindano hayo yatakayofanyika kuanzia Julai 9 hadi 21, mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Akiongoza droo hiyo, Meneja Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema kuwa michuano hiyo imepangwa katika makundi matatu ambapo Kundi A litaundwa na Coastal Union (Tanzania), Ali Wadi FC (Sudan), JKU (Zanzibar) na Dekedaha FC kutoka Somalia.
Kizuguto alisema Al Hilal ya Sudan, Gor Mahia FC (Kenya), Red Arrows FC (Zambia) na Telkom FC (Djibouti) zenyewe ziko katika Kundi B wakati Kundi C linajumuisha SC Villa (Uganda), APR (Rwanda), Singida Black Stars (Tanzania) na El Merriekh Bantui (Sudani Kusini).
Meneja huyo alisema kuwa mechi za mchana zitachezwa kwenye Uwanja mpya wa KMC uliopo Mwenge na zile za usiku zitafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex.
“Kila timu itacheza michezo mitatu na hakutakuwa na michezo ya robo fainali, kwa zile ambazo zitafanya vyema, moja kwa moja zitaingia hatua ya nusu fainali,” alisema meneja huyo.
Aliongeza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na wanaamini mashindano hayo yatasaidia timu za CECAFA kujiandaa na msimu mpya wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.