SERIKALI yaongeza Posho Madaktari Wauguzi
JIUNGE NASI TELEGRAM BOFYA HAPA WHATSAPP BOFYA HAPA
SERIKALI yaongeza Posho Madaktari Wauguzi
SERIKALI yaongeza Posho Madaktari Wauguzi, Serikali ya Tanzania imesema kuwa imeongeza posho za madaktari wanapoitwa nje ya saa za kazi, posho ya sare za wauguzi na ile ya kuchunguza maiti kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miaka mingi imepita tangu madaktari na wauguzi nchini, kuomba ongezeko hilo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akitaja maazimio ya mkutano wa siku tatu wa rasilimali watu ulioandaliwa ndani ya Kumbukizi ya Hayati Benjamin William Mkapa uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam July 31-2024.
“Miongoni mwa maazimio ni pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi tutaendelea kufuata maelekezo yako Rais Samia Suluhu Hassan katika hili.
“Tumeshaanza utekelezaji wa kuongeza ‘OnCall allowance’ za madaktari zilikuwa hazijaongezwa, posho ya sare ya wauguzi, posho ya kuchunguza maiti na nyingine kuanzia Julai hii na hili ulituelekeza,” amesema.
Amesema kuwa miongoni mwa mambo yaliyoibuka katika kongamano hilo ni uzalishaji wa madaktari, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa maabara na kukosekana kwa ajira.
“Madaktari na wataalamu tunazalisha wengi kupitia vyuo vyetu na hatuwapi ajira, lazima tutatue changamoto hii. Tutakaa na mabaraza ya wanataaluma wakiwemo MAT, wafamasia, wauguzi, maabara tukubaliane njia bora ya kudhibiti watumishi wa afya ambao wapo barabarani,” amesema Waziri Ummy.
Amesema miongoni mwa maazimio ni pamoja na kuhakikisha hospitali zinaajiri Watumishi wa mikataba na kwamba mchakato wa bima ya afya kwa wote utakapokamilika utaziwezesha na hospitali za chini kuajiri Watumishi wa mikataba.
Ametaja maazimio mengine kuwa ni kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya, kuendeleza huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa kuwasomesha wataalamu bingwa na bobezi kama ambavyo Serikali imeendela kuwasomesha kupitia mpango wa “Samia Health Super Specialization Program”.