SIMBA Day 2024 Kuzinduliwa Mikumi, Hii Hapa Ratiba Kamili
JIUNGE NASI TELEGRAM BOFYA HAPA WHATSAPP BOFYA HAPA
SIMBA Day 2024 Kuzinduliwa Mikumi, Hii Hapa Ratiba Kamili
SIMBA Day 2024 Kuzinduliwa Mikumi, Hii Hapa Ratiba Kamili,Klabu ya Simba leo imetangaza kuzinduliwa kwa shamrashamra kuelekea Simba Day ambayo kilele chake kutakuwa August 03 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar Es Salaam.
Simba imepanga kuzindua wiki ya Simba 2024 Mkoani Morogoro ambapo Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Imani Kajula amesema kuwa uzinduzi huo utafanyika katika mbuga ya Mikumi.
Kajula amesema kuwa kuna matukio mengi yameandaliwa katika uzinduzi huo ambapo amewataka Wanamsimbazi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu.
“Tunalenga kuzindua Wiki ya Simba Mkoani Morogoro ndani ya Hifadhi ya Mikumi. Simba ni timu ya watu wote ndio maana tumewapa heshima Wanasimba wa Morogoro kufanya uzinduzi na kitovu itakuwa Mikumi tukianza safari kwa muda wa saa 1.”
“Kwenye mbuga ya Mikumi sio tu kufanya uzinduzi na kurudi, kuna uwanja mzuri sana wa mpira na Ahmed atazungusha namba 6, yawezekana pia Ally Kiba akawepo. Mimi nitazungusha namba 10. Ubaya Ubwela hadi kwenye mbuga za wanyama,” alitamba Kajula
“Wiki ya Simba itakuwa na mambo mengi kama kusaidia jamii, kuamsha hamasa ya mashabiki, kuenzi waasisi wa Simba lakini pia michezo ni sehemu ya utalii ndio maana mara nyingi sana Simba tumekuwa tukioanisha mikakati yetu na ya utalii”
Aidha TRC kupitia treni ya mwendo kasi SGR watasafirisha mashabiki kutoka jijini Dar es salaam ambao wangependa kuwa sehemu ya tukio la uzinduzi huo.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa ameishukuru klabu ya Simba kwa kushirikiana nao katika kuhakikisha Wanasimba wanapata usafiri bora na nafuu kuelekea Morogoro.
“Tutashirikiana na ninyi kwa kwenda na kurudi pamoja Morogoro na hata ukiangalia nauli zetu ni rafiki Tsh. 13,000 tu. Tunawashukuru sana kwa tukio hili, ni tukio la kizalendo, kwa sisi SGR ni jambo kubwa tunahitaji kuonekana,” alisema Kadogosa
Nae Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, Agustino Masesa amewakaribisha Wanasimba Mikumi kwenda kushuhudia Wanyama mbalimbali akiwemo Mnyama Simba.
“Simba inakuja Mikumi na Mikumi kuna Simba. Mnakuja kukutana na Simba wa kweli. Tunawakaribisha sana na tunawashukuru sana kwa kutupa heshima ya kuja kuzindulia Simba Week kwenye hifadhi yetu, “alisema Masesa
Kwa Upande wa Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii, Nassor Garamatatu amesema kuwa waingia makubaliano hayo Kwa sababu kubwa mbili, moja kuhamasisha utalii wa ndani na nje kupitia uzinduzi wa Wiki ya Simba na Sababu namba mbili wanafahamu ushawishi Klabu ya Simba.
“Tumeingia ushirikiano huu kwa sababu kuu mbili, moja kuhamasisha utalii wa ndani na nje kupitia uzinduzi wa Wiki ya Simba. Sababu namba mbili tunafahamu ushawishi Klabu ya Simba imekuwa nao kwenye mitandao ya kijamii.Wamefanya kampeni nyingi za aina hii kama ya mwaka jana kwenda Mlima Kilimanjaro na Visit Zanzibar hivyo tunaamini kampeni hii itatoa hamasa kwa Watanzania kwenda kwenye vivutio vilivyo karibu nao kwa kutumia treni ya SGR.”- Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Nassor Garamatatu.
Gharama ya kuingia mbuga ya Mikumi kufanya utalii wa ndani ni Tsh 5,900/- ambapo Msemaji wa Simba Ahmed Ali amewahamasisha Wanamsimbazi kufanya utalii wa ndani
“Twendeni Hifadhi ya Mikumi tukawaonyeshe Watanznia kuna hifadhi, ni karibu na kiingilio ni 5,900. Kuna wengine wakisikia utalii wanajua ni mamilioni kumbe ni hela kidogo. Lakini pia ni kwenda kutangaza treni mpya ya SGR. Kwanza ni bidhaa mpya ambayo inatakiwa kutangazwa na sisi Simba Sports Club ndio Wenye Nchi kuitangaza”
“Safari yetu itakuwa ni Julai 24, 2024 na treni itaondoka Dar es Salaam saa 12:00 alfajiri, muda wa kufika kituoni ni saa 11:00 alfajiri. Wale wote ambao wanatamani kuungana nasi kuelekea Morogoro kufika kwa wakati. Tutafika Morogoro saa 1:30 asubuhi. Mpaka sasa tumekodi behewa tatu kwa ajili ya Wanasimba na kwa mashabiki wetu hakutakuwa na nauli. Kila shabiki wa Simba ambaye anahitaji kuandika historia kupanda SGR, kufika Mikumi, kushiriki uzinduzi wa Wiki ya Simba afike akiwa na jezi ya Simba”
“Tukifika Morogoro tutakuta Wanasimba wenzetu wamekuja kutupokea. Kwa hili niyashukuru matawi ya Simba Morogoro. Tunataka kwenda kuishangaza Morogoro na ninyi mnatujua sisi sio watu wa kufanya mambo madogo madogo, tunafanya kwa ukubwa wake. Na nichukue nafasi hii kuwambia wakati wa Morogoro anayekwenda kazini awahi mapema kabla ya saa 1:30 asubuhi maana Mnyama akifika atakuwa mtaani kufanya hamasa zake.”
“Tutafanya utalii mbugani na baada ya hapo tutacheza mechi tutarudi Morogoro mjini na kuanza sfaari kurudi Dar es Salaam. Hii itakuwa tarehe 24, Julai. Tutakwenda na kurudi lakini kama ukitaka kulala Morogoro unaruhusiwa,” alisema Ahmed
PATA NYIMBO ZOTE MPYA BONYEZA HAPA
MATANGAZO YA BIASHARA WASILIANA NASI KUPITIA nijuzehabariblog@gmail.com
Tags: Hii Hapa Ratiba Kamili, SIMBA Day 2024 Kuzinduliwa Mikumi