TANZIA: Yusuf Manji Afariki Dunia
JIUNGE NASI TELEGRAM BOFYA HAPA WHATSAPP BOFYA HAPA
TANZIA: Yusuf Manji Afariki Dunia
TANZIA: Yusuf Manji Afariki Dunia, Aliyewahi kuwa Muwekezaji wa Klabu ya Yanga SC na Mkurugenzi wa Quality Group Limited (QGL) Bilionea Yusuf Manji amefariki dunia jana Jumamosi Juni 29, 2024 saa 6 usiku katika Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa anapatiwa matibabu akiwa na umri wa miaka 49.
Mtoto wa marehemu, Mehabub Manji amelithibitisha taarifa za kifo cha baba yake akisema baba yake alianza kuungua ghafla na kwenda hospitali sehemu ambayo umauti ulimkuta.
Mwenyekiti huyo wa zamani ambaye alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne akiwa na Yanga na kipindi chote timu ilifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika, anakumbukwa na mashabiki wa timu hiyo kama mmoja kati ya viongozi wenye mafanikio makubwa zaidi Jangwani.
Manji ambaye aliingia madarakani siku chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0 na Simba, Mei 6, 2012 alifanya kazi kubwa kipindi cha uongozi ikiwamo kuhakikisha anavunja makundi mawili makubwa yaliyokuwa yanapingana ndani ya timu hiyo moja likiitwa Yanga Asili na lingine Yanga Kampuni.
Manji aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017, anakumbukwa na Wananchi kwa kufanikiwa kuwasajili wachezaji wakubwa kama Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Emannuel Okwi, Thaabani Kamusoko, Obrey Chirwa na Donald Ngoma kwenye kikosi chake.
Mfanyabiashara huyo ambaye alijiuzulu uenyekiti Yanga, Mei 21, 2017 katika mahojiano yake ya hivi karibuni alisema kuwa anaamini Simba kwa sasa inashindwa kufanya vizuri baada ya kufariki dunia kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Pope ambaye aliamini alikuwa na ubora wa hali ya juu kutambua wachezaji mahiri sokoni.