YANGA Yataja Malengo Matatu 2024/2025
JIUNGE NASI TELEGRAM BOFYA HAPA WHATSAPP BOFYA HAPA
YANGA Yataja Malengo Matatu 2024/2025
YANGA Yataja Malengo Matatu 2024/2025,Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamesema malengo yao kuelekea msimu mpya wa mashindano wa mwaka 2024/2025 ni kufika hatua ya Nusu fainali, Fainali au kubeba taji la Afrika.
Msimu uliopita Yanga ilitolewa katika hatua ya robo Fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kuwa jeuri ya kuzungumza matarajio hayo wanaipata kutokana na kikosi kilichopo, na kile ambacho watakiongeza kuelekea msimu ujao
Kamwe amesema kuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kubakisha wachezaji tegemeo, hivyo kikosi kitakuwa na makali zaidi kwa sababu kitaundwa na nyota wale wale lakini watakiboresha kwa kuongeza wengine ambao wana viwango vikubwa zaidi na kuifanya timu hiyo kuwa tishio
“Kwanza tumefanikiwa kumbakisha Kocha Miguel Gamondi, hiyo peke yake ni jambo kubwa sana, lakini tumewabakisha wachezaji wetu tegemeo ambao walituheshimisha msimu uliopita”
“Kama vile haitoshi tunaongeza na mashine nyingine. Nimechungulia majina ya wachezaji wapya, ni hatari, yaani msimu ujao mbali na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA, tuna malengo mengine matatu”
“Kwanza kabisa ni akili yetu ni kutwaa ubingwa wa Afrika, kama tukishindwa basi tufike fainali tu, na kama ikishindikana tuishie nusu fainali,” alisema Kamwe: YANGA Yataja Malengo Matatu 2024/2025
Kamwe amesema mafanikio hayo itakuwa ni heshima kubwa kwa Yanga kwa sababu haijawahi kufikia hatua hiyo tangu mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), yalipoanzishwa
“Tulikuwa hatujaingia hatua ya makundi kwa miaka 24 hivi, tukaingia na msimu huo huo tukafika robo fainali ambayo tulikuwa hatujawahi kufika tangu mfumo huu wa makundi uanze, na huu ulikuwa msimu mmoja tu, sasa msimu wa pili tunahitaji tuvunje rekodi yetu wenyewe, tukifika nusu fainali tu tutakuwa tayari tumeshafanya hivyo”
“Chochote kikitokea baada ya hapo ni mafanikio, lakini bado ikitokea tukienda fainali ni moja ya malengo tuliyojiwekea na kuchukua ubingwa pia ikiwezekana, hilo kwetu linawezekana kutokana na kikosi tutakachokijenga msimu ujao,” Kamwe alisema