KIKOSI Cha Simba Kitakavyokuwa 2024/2025
KIKOSI Cha Simba Kitakavyokuwa 2024/2025
KIKOSI Cha Simba Kitakavyokuwa 2024/2025,Klabu ya Simba inataka kuhakikisha inamaliza usajili kabla ya Julai 01-2024 kwaajili kwendi nchini Misri kuweka kambi maalumu ya msimu mpya wa 2024/2025 ‘Pre Season’ ikiwa na jeshi lake kamili kuanzia benchi la ufundi na mastaa wake wote.
Hadi sasa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara 22, wamekamilisha usajili wa wachezaji wasiopungua watatu, lakini pia wanaendelea kuwapa ‘Thank You’ baadhi ya nyota waliokuwepo kikosini hapo kwa msimu uliopita sambamba na kuwaongezea mikataba Wachezaji wengine.
Siku chache zilizopita Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori alikuwa Zambia kwenda kumalizana na winga, Joshua Mutale kutoka Power Dynamos ambaye tayari yupo Dar es Salaam kukamilisha mipango ya usajili ikiwemo kutambulishwa.
Pia kiungo Debora Fernandes Mavumbo kutoka Mutondo Stars naye dili lake na Simba lipo hatua za mwisho akiwa tayari amefika hapa nchini akifungiwa kwenye moja ya hoteli ya kifahari.
Lakini pia Simba ilimtambulisha beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Pia Simba ipo mbioni kumtambulisha kiungo Omary Abdallah Omary kutoka Mashujaa FC ya Kigoma na Yusuf Kagoma kutoka Singida Fountain Gate.
Hapo watakuwa wemefika wachezaji watano wapya ambao mambo yasipobadilika msimu ujao watakipiga Msimbazi.
Mwingine ni mshambuliaji Steven Mukwala kutoka Uganda ambaye msimu uliopita alikuwa akikipiga Asante Kotoko na muda wowote kuanzia sasa atatua nchini kusaini mkataba kwani makubaliano ya kila kitu yamefikiwa.
Wakati hayo yakiendelea, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’, yuko nchini DR Congo na inaelezwa ameenda kukamilisha usajili wa wachezaji wawili.
Kuna beki wa kati, Nathan Idumba Fasika aliyewahi kuvitumikia Vilabu vya Valerenga ya Norway, Cape Town City (Afrika Kusini) na FC Saint Eloi (DR Congo).
Mwingine ni winga, Elie Mpanzu kutoka AS Vita Club na kama atafanikiwa basi atarudi nao nchini kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda Misri kuweka kambi.
Simba pia ipo kwenye mazungumzo mazuri na kiungo mkabaji, Agustine Okejepha kutoka Rivers United ya Nigeria na huenda wakafikia muafaka wa kusaini mkataba.
Okejepha raia wa Nigeria, anatajwa kama mrithi sahihi wa Sadio Kanoute aliyemaliza mkataba huku ikielezwa hana mpango wa kusalia kikosini hapo sambamba na Babacar Sarr anayetajwa kuwepo kwenye mikakati ya kuvunjiwa mkataba ingawa bado pande zote mbili hazijafika muafaka.
Tayari Simba imeachana na Shaban Chilunda, John Bocco, Saido Ntibazonkiza, Henock Inonga, Luis Miquissone na Kennedy Juma, huku wengine wengi wakitarajiwa kuagwa muda wowote.
WANNE UHAKIKA
Nyota wanne ambao mikataba yao ilikuwa ukingoni kumalizika ndani ya kikosi hicho, tayari wameongezewa hivyo wana uhakika wa kuendelea kuitumikia Simba kwa msimu ujao.
Watatu kati ya hao wameshatambulishwa rasmi ambao ni Kibu Denis, Israel Mwenda na Mzamiru Yassin, huku Shomari Kapombe ambaye inaelezwa amepewa mwaka mmoja naye atatangazwa muda wowote.
BENCHI LA UFUNDI
Msimu uliopita Simba ilimaliza na Juma Mgunda ambaye alikuwa Kaimu Kocha Mkuu akichukua mikoba ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka mwezi Aprili.
Mgunda alikuwa akisaidiana na Seleman Matola ambapo walipambana na timu hiyo ikashika nafasi ya tatu katika Msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Taarifa zilizopo hivi sasa ni kwamba, Mgunda mkataba wake na Simba umemalizika, lakini hata hivyo mipango iliyopo muda mrefu ni kusaka kocha mwingine ambaye ataiongoza timu hiyo msimu ujao watakapoenda kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na ile ya ndani ikiwemo Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA) na Ngao ya Jamii.
Kutokana na hilo, Simba wamepanga kabla ya kufika Ijumaa, wawe wamemtambulisha kocha wao mpya ambaye atakuja kuungana na jeshi lake hilo jijini Dar es Salaam kwani mikakati iliyopo ni kwamba kuanzia leo Alhamisi Wachezaji wataanza kuwasili kambini ili kesho Ijumaa wakutane na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye pia ni Rais wa Heshima wa Klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’ kwaajili ya kuweka mikakati sawa kabla ya kwenda kuanza Pre Season.
Kocha anayepewa nafasi zaidi ni Msauzi, Steve Kompela ambaye taarifa zilizopo zinabainisha kuwa walifanya naye mawasiliano hapo awali. Wengine watakaoongezeka katika benchi la ufundi ni kocha wa viungo, kocha wa makipa na meneja wa timu ambaye anatajwa kurudishwa kundini Patrick Rweyemamu.
KIKOSI KITAKAVYOKUWA
Kama mambo hayatabadilika, basi Simba katika kikosi chao cha msimu ujao kitakuwa na maingizo mapya si chini ya nane ikiwa ni mchanganyiko wa wazawa na kimataifa ambao ni Nathan Fasika Idumba, Debora Fernandes Mavumbo, Agustine Okejepha, Joshua Mutale, Steven Mukwala, Elie Mpanzu, Lameck Lawi, Omary Abdallah Omary na Yusuf Kagoma.
Kikosi kitasomeka hivi;
- Ayoub Lakred
- Israel Mwenda
- Mohamed Hussein
- Che Malone Fondoh
- Fasika Idumba
- Agustine Okejepha
- Joshua Mutale
- Debora Mavumbo
- Steven Mukwala
- Kibu Denis na
- Eli Mpanzu.
Akiba watakuwa ni;
- Aishi Manula
- Shomari Kapombe
- Omary Abdallah Omary
- Aubin Kramo
- Mzamiru Yassin
- Fabrice Ngoma na
- Yusuf Kagoma.
Soma zaidi: KIKOSI Cha Simba Kitakavyokuwa 2024/2025