KATIBA Ya Chama Cha Mapinduzi 1977 Toleo la Desemba 2022
KATIBA Ya Chama Cha Mapinduzi 1977 Toleo la Desemba 2022
KATIBA Ya Chama Cha Mapinduzi 1977 Toleo la Desemba 2022, Toleo hili limezingatia na kuweka pamoja marekebisho yote yaliyofanywa katika Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya 1977, Toleo la 1980, 1982, 1984, 1987, 1990, Machi (1992), Septemba (1992), 1994, 1995, 1997, 2005, 2007, 2012, 2017 , 2020, Aprili (2022) na Desemba (2022).
KATIBA YA CHAMA CHA MAPINDUZI
AZIMIO LA MKUTANO MKUU WA TAIFA WA PAMOJA WA TANU NA ASP
Kwa kuwa Mkutano Mkuu wa Taifa wa pamoja, kwa niaba ya Wana TANU na Wana ASP, kwa pamoja tunaelewa na kukubali kwamba jukumu letu katika Historia ya Taifa ni kuimarisha Umoja, kuleta Mapinduzi ya Kijamaa Tanzania na kuendeleza mapambano ya Ukombozi katika Afrika na kote Duniani;
Kwa kuwa tunatambua kuwa Mapambano ya Kujenga Ujamaa katika Tanzania na kushiriki kwetu kwa ukamilifu katika harakati za Mapinduzi ya Afrika na Dunia kunahitaji Chombo madhubuti cha uongozi kinachounganisha fikra na vitendo vya Wafanyakazi na Wakulima;
Kwa kuwa tunazingatia na kuthamini kazi nzuri ya kimapinduzi na ya mafanikio makubwa iliyokwishafanywa na TANU na ASP katika kumwondoa Mwafrika kutoka kwenye unyonge wa kunyonywa, kunyanyaswa na kudharauliwa na kumfikisha kwenye uhuru na kuheshimiwa;
Kwa kuwa tunatambua kuwa Umoja wa TANU na ASP unatokana na ushirikiano wetu wa miaka mingi tangu wakati wa Mapambano ya kupigania Uhuru hadi sasa, na unatokana pia na Siasa yetu moja ya Ujamaa na Kujitegemea;
Kwa kuwa tunatambua pia kwamba kuweko kwa Vyama viwili katika mazingira ya Chama kimoja cha Siasa kunapunguza upeo wa Nguvu na Umoja wetu katika kuendeleza mapambano ya kujenga Ujamaa nchini na kushiriki kwa pamoja kwa ukamilifu katika harakati za Mapinduzi ya Tanzania, ya Afrika na ya Dunia;
Kwa kuwa, kihistoria, tumeongozwa na kumbukumbu ya kitendo kama hiki cha kimapinduzi na busara ambacho Waanzilishi wa TANU, chini ya Uongozi wa Mwalimu Julius K. Nyerere walikifanya hapo awali cha kuvunja Chama cha African Association na kuunda TANU, na waanzilishi wa ASP chini ya uongozi wa Marehemu Abeid Amani Karume, walikifanya hapo awali cha kuvunja Vyama vya African Association na Shiraz Association na kuunda ASP, shabaha yao wote ikiwa ni kuunda Chama kipya madhubuti na cha kimapinduzi chenye uwezo mkubwa zaidi wa kuongoza mapambano ya wananchi wetu katika mazingira mapya ya wakati huo. Kwa hiyo basi:
Sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa pamoja wa TANU na ASP tuliokutana leo tarehe 21 Januari, 1977 mjini Dar es Salaam, chini ya uongozi wa pamoja wa Mwalimu Julius K. Nyerere Rais wa TANU na Ndugu Aboud Jumbe, Rais wa ASP, kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari 1977 na wakati huo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.
Vyama vya TANU na ASP vinavunjwa kwa taadhima kubwa. TANU na ASP havikuamua kujivunja kama vyama kwa kuwa vimeshindwa kutekeleza jukumu lao. Kwa hakika TANU na ASP ni Vyama vilivyopata mafanikio ya kipekee katika Afrika katika kulitekeleza jukumu la
Kihistoria na mafanikio hayo ndiyo leo yamewezesha kitendo hiki cha Vyama viwili kujivunja vyenyewe. TANU na ASP vitaheshimiwa siku zote kama viungo muhimu katika Historia ya Mapambano ya Ukombozi wa Taifa letu na wa Bara la Afrika, na waanzilishi wa TANU na ASP watakumbukwa daima kama mashujaa wa taifa letu waliotuwezesha leo kupiga hatua hii ya kufungua ukurasa mpya katika Historia ya Tanzania.
Tumeamua kwa pamoja kuunda Chama kipya cha kuendeleza mapinduzi ya kijamaa nchini Tanzania na Mapambano ya Ukombozi wa Afrika juu ya misingi iliyojengwa na TANU na ASP.
Chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini, na kupambana na jaribio lolote lile la mtu kumuonea mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au kuzorotesha maendeleo ya Taifa;
Chama tunachokiunda tunataka kishike barabara hatamu za uongozi wa shughuli zote za umma kwa maslahi ya Wafanyakazi na Wakulima wa Taifa letu;
Chama tunachokiunda tunataka kiwe kiungo kati ya Wanamapinduzi wa Tanzania na Wanamapinduzi wenzetu kokote waliko.
BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD PDF YA KATIBA CCM JANUARY 2023
Tags: KATIBA Ya Chama Cha Mapinduzi 1977 Toleo la Desemba 2022