MAKOCHA Wanaotajwa kurithi Mikoba ya Benchikha Simba
MAKOCHA Wanaotajwa kurithi Mikoba ya Benchikha Simba
MAKOCHA Wanaotajwa kurithi Mikoba ya Benchikha Simba, Klabu ya Simba imeanza mchakato wa kutafuta Kocha mpya atakayerithi mikoba ya Abdelhak Benchikha ikipanga kukamilisha suala hilo kabla ya msimu huu kumalizika.
Viongozi wa Simba walikaa kikao na Kwa pamoja waliamua kuanza mara moja mchakato wa kupata mrithi wake ambaye atainoa walau mechi tatu za mwisho wa msimu huu, ili ajue wapi pa kuanzia katika usajili dirisha kubwa litakapofunguliwa.
Simba inataka kocha atakayewajengea uwezo wachezaji na kupata timu itakayocheza kwa muunganiko, umoja na mshikamano bila kuwa na matabaka.
Sifa nyingine ambayo Simba inaizingatia kupata kocha mpya ni lazima awe na uzoefu wa kutosha kwenye soka la Afrika, hususan katika michuano ya CAF ambayo timu hiyo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiishia Robo Fainali.
Miongoni mwa makocha wanaotajwa kurithi mikoba ya Benchikha ni Lamine N’Diaye ambaye kwa sasa ni kocha wa TP Mazembe, lakini kabla ya hapo aliwahi kuzinoa Horoya ya Guinea, Al Hilal ya Sudan, Maghreb de Fes ya Morocco, Coton Sports ya Cameroon na timu ya taifa ya Senegal.
Kocha huyo msimu huu ameifikisha TP Mazembe hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ukiwa ni msimu wake wa kwanza.
Mwingine ni Alexandre Santos, kocha Mkuu wa Petro de Luanda ya Angola ambayo msimu huu imetolewa katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha huyo pia aliwahi kuwindwa na Simba mwaka 2022, lakini dili lake halikukamilika.
Mwingine ni Omar Najhi ambaye alizidiwa kete na Benchikha kwani alikuwa kwenye rada za Simba wakati alipofukuzwa Oliveira Roberto ‘Robertinho’.
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha Wydad Casablanca na Mouloudia za Morocco kwa sasa yupo huru baada ya kuchana na Ittihad Tanger ya nchini humo.
Hao ni baadhi ya makocha ambao inaelezwa wapo kwenye listi ndefu iliyopo mezani kwa Simba huku Juma Mgunda naye akifikiriwa kubakizwa kikosini hapo kama kocha Msaidizi endapo watapata Kocha Mkuu.
Kwa sasa Simba ipo chini ya Mgunda anayekaimu nafasi ya Kocha Mkuu akisaidiwa na Selemani Matola ni Mchezaji wa zamani wa Timu hiyo.