COPCO FC Mabingwa Fahari Super Cup 2024
COPCO FC Mabingwa Fahari Super Cup 2024
COPCO FC Mabingwa Fahari Super Cup 2024, Timu ya Copco Football Club ya Buswelu Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mweta Sports Club ya Kisesa Wilayani Magu katika uwanja wa Red Cross Kisesa.
Akizungumzia baada ya kumalizika mtanange huo Mgeni Rasmi Mheshimiwa, Mary Francis Masanja ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum alisema kuwa amefarijika na vipaji vya timu zote na kuomba uongozi wa timu hizo kuvisaidia vipaji hivyo ili vilete faida kwa wahusika na taifa kwa ujumla.
“Nimefarijika na michuano hii, nimependa vipaji vya wachezaji. Hakika kuna vipaji vingi na vizuri sana. Vijana wanajua sana na wana vipaji na uzuri bado wana umri mdogo. Wakiendelezwa watakuwa na faida kwa timu zetu za taifa na wao wenyewe kujiletea vipato”
Aidha Mheshimiwa Masanja amewaasa wana Mwanza kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa CCM Kirumba tarehe 10, 2024 kushuhudia timu yao ya Pamba Jiji FC ambao ndio Fahari ya Mwanza na Kanda ya Ziwa.
“Nitoe wito kwa wana Mwanza na Kanda ya Ziwa, wajitokeza kwa wingi uwanja wa CCM Kirumba tarehe 10, 2024 kuiona timu yao Pamba Jiji FC. Ni timu ya wana Mwanza na Kanda ya Ziwa na tunajivunia kuwa nayo. Tafadhali nunueni tiketi mapema wote ili mje kupata raha ya Pamba”
Mratibu wa michuano hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Mweta Sports Centre, Wilbert Mweta amesema kuwa michuano hiyo kwa msimu huu ilikuwa mizuri na kuwaasa wachezaji wote kuendelea kujituma ili wafikie lengo kamili ya kuwa wachezaji wakubwa.
Copco Football Club imetwaa Kombe pamoja na zawadi ya shilingi milioni moja na medali, huku Mweta Sports Club wakipata zawadi wa shilingi laki tano na medali.
Huu unakuwa msimu wa tatu kwa michauno hiyo ya Fahari Super Cup, ambayo kwa msimu miwili ya mwanzo kombe lilichukuliwa na Mweta Sports Club.