DARAJA la J.P Magufuli Kigongo Busisi kurahisisha Usafiri
Daraja la J.P Magufuli la Kigongo Busisi linalojengwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) jijini Mwanza imeelezwa kuwa litarahisisha usafiri na usafirishaji kwa mikoa na nchi za jirani.
Msimamizi wa mradi huo wa kimkakati, Mhandisi Devotha Kafuku amesema hayo leo tarehe 22 Agosti, 2024 kwenye kongamano na Maonesho ya Tisa ya Wahandisi Wanawake Tanzania (TAWECE) yanayofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Kafuku amesema kuwa, daraja hilo lenye urefu wa Kilometa tatu (KM 3) ni daraja la kwanza kwa urefu zaidi kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati na la sita kwa dunia nzima, litakapokamilika litaunganisha wilaya mbili za Misungwi na Sengerema, na pia litaunganisha barabara zote za mikoa iliyopo kandokando mwa Ziwa Victoria jijini hapo.
“Hili daraja limejengwa kimkakati na sio litaunganisha tu hizi wilaya, bali litakwenda kuunganisha barabara inayoelekea mpakani mwa Sirari na kwenda hadi Mtukula mpaka wa kwenda Uganda; pia Rusumo ambayo ni mpaka wa kwenda nchi ya Rwanda, Kabanga, Burundi, Kigoma kwenda Congo,” amesema Mhandisi Kafuku.
Ameongeza kuwa, daraja hilo ni muhimu kwa kuwa litakuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa mikoa yote ya kanda ya ziwa na kwa wananchi mmoja mmoja.
Vilevile amesema, daraja hilo likikamilika litarahisisha usafiri kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, ambapo watatumia muda mfupi kutoka wilaya moja kwenda nyingine, kwa kuwa sasa wanatumia usafiri wa vivuko vyenye kutumia muda mrefu.
“Kwa sasa tunatumia vivuko, na mwananchi akipanda kivuko kutoka Misungwi na kwenda Sengerema anatumia takribani saa tatu hadi nne, lakini daraja likikamilika wataweza kutumia dakika tatu hadi nne kuvuka na hakutakuwa na muda wa kusubiri kwa kuwa muda ni mali na mtu anapookoa muda maana yake anaokoa hata maendeleo yake binafsi,” amesema Mhandisi Kafuku.
Aidha, ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika kujenga daraja hili, ambalo liliasisiwa na Hayati Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli ambapo hadi anafariki tarehe 17 Machi, 2021 ujenzi wake ulikuwa umefikia asilimia 25.
Tags: DARAJA la J.P Magufuli Kigongo Busisi kurahisisha Usafiri