TAKUKURU Yaokoa Zaidi ya Milioni 4.3 za Wanufaika wa TASAF Ngara
TAKUKURU Yaokoa Zaidi ya Milioni 4.3 za Wanufaika wa TASAF Ngara
TAKUKURU Yaokoa Zaidi ya Milioni 4.3 za Wanufaika wa TASAF Ngara, Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kuokoa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi milioni 4.3 za wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF 139 katika wilaya ya Ngara.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Manispaa ya Bukoba Agosit 6 mwaka huu 2024, Naibu Mkuu wa Takukuru Ezekia Sinkala amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Machi hadi juni taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa kiasi hicho cha fedha baada ya kupokea taarifa ya ubadhilifu kwenye kijiji cha Kumutana kata ya Kibimba Wilayani Ngara.
Hata hivyo Sinkala amesema kuwa baada ya kufanyika uchunguzi ilibainika mnamo mwezi Septemba 24 mwaka 2020 kulikuwa na zoezi la uhalalishaji wa fedha za TASAF katika kijiji hicho za kipindi cha mwezi mei hadi juni na mwezi julai hadi Agosti yaani mgao wa madirisha mawili kwa wanufaika.
“Katika ufatiliaji ilibainika kwamba fedha husika zilizochukuliwa na kupelekwa kijiji cha kumutana zilikuwa jumla ya shilingi milioni 9,332,000 kwa awamu zote mbili yani kiasi cha shilingi milioni 4,666,000 kwa kila awamu lakini kwa makusudi wasimamizi walitumia uelewa mdogo wa wanufaika na kuwalipa fedha ya awamu moja badala ya mbili”alisema Sinkala.
Naibu huyo Sinkala amesema wasimamizi walirejesha sehemu ya fedha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara ambapo fedha hizo walirejeshewa wananchi pamoja na kurejeshwa kwa fedha hizo wasimamizi husika walishindwa kurejesha kiasi cha fedha kilichobaki na kukana kuhusika na ubadhirifu huo hadi ulipofanyika uchunguzi na kuthibitika kuwa ni kweli walilipa awamu moja badala ya mbili.
Aidha wanakijii cha Kumtana wameishukuru taasisi hiyo na Serikali kwa ujumla kwa kufanikisha kurejeshewa fedha zao ambazo zilidhulumiwa na kuhaidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutokomeza vitendo vya rushwa wilayani humo.
Tags: TAKUKURU Yaokoa Zaidi ya Milioni 4.3 za Wanufaika wa TASAF Ngara