SIMBA vs APR FC Simba Day August 03-2024
SIMBA vs APR FC Simba Day August 03-2024
SIMBA vs APR FC Simba Day August 03-2024, Mabingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda, Klabu ya APR FC ndio watakuwa wageni wa Simba katika sherehe za kilele cha siku ya SIMBA DAY zitazofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es salaam Agosti 3,2024.
Tamasha hilo la kila mwaka linawakutanisha wanachama na mashabiki wa Simba ambao pamoja na mambo mengine ya burudani ya muziki na ngoma kutoka kwa wasanii mbalimbali pia kunakuwa na mechi za timu za vijana na za wanawake.
Pia Simba hutumia tamasha hilo kutangaza kikosi kipya kwaajili ya mashindano mbalimbali Msimu unaofuata na baadae kumalizia tamasha hilo kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki.
Kilele hicho kinatanguliwa na wiki nzima ya wanachama na mashabiki kufanya kazi za kijamii maeneo mbalimbali nchini kabla ya wote kujumuika Uwanja wa Mkapa kwenye siku ya kilele ambapo watacheza dhidi ya Mabingwa wa Rwanda APR FC.
Tamasha hilo litakuwa la 25 kwa klabu hiyo kubwa tangu walipobuni na kulifanya kwa mara ya kwanza mwaka 2009 chini ya Mwenyekiti wa Klabu hiyo wakati huo, Hassan Dalali, ambapo sasa imekuwa ni utamaduni wao kufanya tamasha hilo.
Miaka michache baada ya kuanzisha tamasha hilo, klabu nyingine nazo zilianza kufanya matamasha yao.
Katika tamasha la kwanza mwaka 2009, Simba ilicheza mechi kirafiki na klabu ya SC Villa ya Uganda kwenye Uwanja wa Uhuru na ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Hilary Echessa, kiungo wa Kenya aliyekuwa amesajliwa msimu huo, timu ikiwa chini ya kocha Mzambia, Patrick Phiri.
Ni msimu huo Simba ilikuwa imewasajili kwa mara ya kwanza wachezaji wawili raia wa Uganda, Emmanuel Okwi na Joseph Owino.
Tamasha la msimu uliopita lilifanyika Agosti 6, Uwanja wa Benjamin Mkapa Simba ikicheza dhidi ya Power Dynamos ya Zambia na kupata ushindi wa mabao 2-0 yaliyowekwa wavuni na Willy Onana na Fabrice Ngoma ambao nao walikuwa wachezaji wapya katika kikosi hicho.