WASIFU wa Hayati Yusuf Manji
WASIFU wa Hayati Yusuf Manji
WASIFU wa Hayati Yusuf Manji, Mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji amefariki dunia Jumamosi ya Juni 29, 2024 katika Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa anapatiwa matibabu.
Mtoto wa marehemu, Mehabub Manji alilithibitisha kifo cha baba yake akisema alianza kuugua ghafla na kwenda hospitali sehemu ambayo umauti ulimkuta.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Yanga alifanikiwa kuchukua Ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne 2012/2013 na mara tatu mfululizo 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017.
Pia, alifanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho FA na Kombe la Kagame 2012 likiwa ndiyo kombe la mwisho la michuano hiyo kwa Yanga.
Akiwa na Yanga kipindi chote timu ilifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ingawa haikufanya vizuri sana, anakumbukwa na mashabiki wa timu hiyo kama mmoja kati ya viongozi wenye mafanikio makubwa zaidi Jangwani lakini akiwa mmoja kati ya watu walioleta mapinduzi ya soka Tanzania.
Manji aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017 baada ya kukwaruzana na wazee wa timu hiyo akiwemo marehemu Yahaya Akilimali.
Mara baada ya Manji kujiuzulu klabu hiyo ilipita kwenye ukata mkubwa ambapo ilianza kutembeza bakuli kwaajili ya kujiendesha ambapo lilipewa jina la Kubwa Kuliko na kuhamishia utawala wa soka la Tanzania kwa Simba ambayo ilitwaa ubingwa wa ligi mara nne mfululizo na Azam mara moja, hadi timu hiyo ilipopata uwekezaji wa GSM ndipo ikarejea kwenye makali yake ya kutwaa Ubingwa mara tatu mfululizo hadi msimu uliopita.
WASIFU WA HAYATI YUSUF MANJI
Alizaliwa Oktoba 14, 1975 katika Jiji la Dar es Salaam, Tanzania
Mwaka 1995 alianzisha kampuni ya Quality Group Limited iliyofahamika Tanzania na Afrika kwa kusambaza bidhaa mbalimbali.
Alisoma shahada ya uhasibu kutoka Chuo cha Hofstra kilichopo jiji la New York, Marekani.
Mwaka 2015, alichaguliwa kuwa Diwani wa Mbagala Kuu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
Enzi za uhai wake, Manji alifanikiwa kupata watoto wawili
Aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017.
Amefariki dunia Juni 29, 2024 Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa akipatiwa matibabu.
Manji amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 49.