WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Azindua Uboreshaji wa Daftari Ia Kudumu Ia Wapiga Kura Kigoma awataka raia wote……
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Azindua Uboreshaji wa Daftari Ia Kudumu Ia Wapiga Kura Kigoma awataka raia wote……
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Azindua Uboreshaji wa Daftari Ia Kudumu Ia Wapiga Kura Kigoma awataka raia wote……,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) amezindua Uboreshaji wa Daftari Ia Kudumu Ia Wapiga Kura leo tarehe 20 Julai, 2024 Mkoani Kigoma na kushuhudia kuandikishwa kwa Mpiga Kura na Kumkabidhi kadi yake.
Akihutubia Wananchi waliohudhuria hafla ya Uzinduzi huo uliyofanyika uwanja wa Kawawa uliopo Halmashuauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Mhe. Majaliwa amewataka raia wote wa Tanzania wenye sifa wajitokeze kujiandikisha kuwa wapiga kura na kuhakikisha kuwa wasio raia wa Tanzania hawaandikishwi kwenye Daftari Ia Kudumu Ia Wapiga Kura.
Amesisitiza kuwa kuwa zoezi hilo ni kwaajili ya maandalizi ya uchaguzi na kwamba wasio raia wa Tanzanai hawahusiki.
“anayetakiwa kaundikishwa hapa ni raia wa Tanzania tu. Hapa ni lazima tuwe wazalendo. Tusiruhusu mtu yeyote kutoka nje kujiandikisha kuwa mpiga kura,” amesema.
Mhe. Majaliwa pia amevitaka vyama vya siasa kutumia ruhusa ya kisheria ya kuweka mawakala kila kituo, kuhakikisha wanachagua mawakala ambao wanatoka kwenye maeneo vilipo vituo vya kuandikisha wapiga kura ili wawaze kuwatambua watu wanaojiandikisha na uraia wao.
“Mawakala wa vyama vya siasa mnaowajibu wa kuwatambua wanaojiandikisha, naomba nisisitize hapa, lazima muwe wazalendo namba moja, uzalendo wenu utasaidia kuwatambua watu ambao sio raia.”
Akizungumzia ushiriki wa vijana katika uboreshaji, Mhe. Majaliwa amewataka vijana waliofikia umri wa kupiga kura shime, kutumia fursa ya uboreshaji kujiandikisha kuwa wapiga kura ili wakati wa uchaguzi ukifika watumie haki hiyo kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Ili kuhakikisha uboreshaji unafanyika kwa amani, Mhe. Majaliwa alilikumbusha Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha linaimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ambayo uboreshaji utafanyika kuanzia katika Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.
”Katika utekelezaji wa majukumu hayo, epukeni matumizi ya nguvu kupita kiasi zinazoweza kuhatarisha usalama kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura.” Amesema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wa vyombo vya habari, Mhe. Majaliwa alitoa pongezi kwao kwa kazi nzuri na muhimu ya kuuhabarisha umma tangu hatua za mwanzo za maandalizi ya zoezi hili linaloanza leo.
Hata hivyo, aviwasisitiza vyombo vya habari viendelee kutoa habari sahihi na zilizofanyiwa utafiti kuhusu zoezi hili muhimu kwa nchi yetu.
Mhe. Majaliwa amewasihi wazee wa kimila watumie ushawishi wao katika jamii, kuwahimiza watu wenye sifa kwenye jamii wanazoziongoza, wajiandikishe kuwa wapiga kura au kuboresha taarifa zao ili ifikapo mwaka 2025 waweze kupiga kura ya kumchangua Rais, Mbunge na Diwani.
Kwa upande wa viongozi wa dini.Mhe. Majaliwa amewataka viongozi hao kutumia majukwaa ya Misikiti na Makanisa kuwahimiza na kuwakumbusha waamini na waumini wao wajitokeze kujiandikisha kuwa wapiga kura.
“Vilevile, endeleeni kuhamasisha waumini wenu waliopoteza kadi au kadi zao zimeharibika pamoja na wale wanaotaka kuboresha taarifa zao binafsi au kuhama kituo kwa pamoja watumie muda huu kwenda kwenye vituo kwaajili ya kuboresha taarifa zao na kukamilisha taratibu zilizowekwa”, amesema Mhe. Majaliwa.
Amesisitiza kuwa kupitia ushiriki wa wadau mbalimbali wa uchaguzi kwamba ana hakika kuwa Tume itaweza kufikia lengo ililojiwekea la kuwa na wapiga kura 34,746,638.
“Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira mazuri kwa wananchi kujitokeza kwa wingi na kutumia vema muda wa siku saba zitakazotumika kwa kila kituo cha kuandikisha wapiga kura.” amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha amewasihi wananchi wa mikoa ambayo zoezi la uboreshaji linaanza kwa mzunguko wa kwanza, yaani mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora, kujitokeza wa wingi.
“Tume imechagua kuanza na mikoa yenu hivyo tumieni fursa hii kujitokeza kwa wingi kuandikishwa kuwa wapiga kura. Jitokezeni kwa wingi kwenye vituo kuanzia leo tarehe 20 Julai, 2024 hadi tarehe 26 Julai, 2024 ambayo ni kilele cha zoezi hilo.” Amesema Mhe. Majaliwa.
Ametoa wito kwa mikoa inayofuata ambayo ni Geita na Kagera, kisha Mwanza, Shinyanga na baadae Mara, Simiyu na sehemu ya Mkoa wa Manyara, wajiandaeni ili tarehe ikifika wajitokeze kwa wingi kutimiza haki yao ya kujiandikisha ama kuboresha au kuhamisha taarifa zao.
Naye Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele amesema Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika katika mizunguko (routes) 13 na leo ndiyo unaanza mzunguko wa kwanza utakaohusisha mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi.
”Zoezi la uboreshaji kwa kila mzunguko (route) litadumu kwa muda wa siku saba ambapo vituo vya kuandikisha vitafunguliwa saa mbili kamili (2:00) asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni ya kila siku kwa kila kituo.”, amesema Mhe. Mwambegele.
Amesema kwa upande wa Zanzibar, zoezi hilo litafanyika kuanzia tarehe 07 hadi 13 Oktoba, 2024, na kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13 (1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 uboreshaji wa Daftari utamhusu mtu yeyote aliyepo Zanzibar ambaye hana sifa za kuandikishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) lakini anayo sifa ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Amefafanua kuwa jumla ya vituo 40,126 vitatumika katika zoezi la uboreshaji wa Daftari. Kati ya hivyo, vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Tanzania Zanzibar. Idadi hii ya vituo ni ongezeko la vituo 2,312 zaidi ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha Wapiga Kura kwa mwaka 2019/2020.
”Kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022, tunatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 5,586,433 ambao wametimiza umri wa miaka 18 na ambao watatimiza umri huo kabla au ifikapo siku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.”, ameeleza na kufafanua kuwa:
“Sanjari na hao tunatarajia wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa kwenye Daftari kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, kukana uraia au kupoteza sifa za kuendelea kuwemo kwenye Daftari.”
Mhe. Jaji Mwambegele ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kifungu cha 10 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, uboreshaji wa mwaka huu utahusisha wafungwa / wanafunzi wanaotumikia kifungo cha chini ya miezi sita na mahabusu waliopo kwenye magereza Tanzania Bara na Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar.