YANGA Yawakana Waliofungua Kesi
YANGA Yawakana Waliofungua Kesi
YANGA Yawakana Waliofungua Kesi,Klabu ya Yanga imesema kuwa waliofungua kesi ya kikatiba dhidi ya Baraza la Wadhamini wao si wanachama wao.
Sambamba na hilo, klabu hiyo imedai saini za baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini zimeghushiwa, hivyo inaangalia utaratibu wa kisheria wa kwenda kushtaki na ikibainika sheria ichukue mkondo wake.
Yanga pia imesema kuwa imegundua kuna baadhi ya watu wasioitakia mema klabu wapo nyuma ya wale waliofungua shauri ili kuung’oa uongozi madarakani.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Wakili wa klabu hiyo, Simon Patrick, alisema wamegundua kesi iliyoendeshwa dhidi ya Baraza la Wadhamini, ilikuwa ni ya upande mmoja, huku pande hiyo ikijigawa na kujifanya ipo upande wa walalamikiwa.
Alisema hayo kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam kutoa amri uongozi wa Yanga, ukiongozwa na Rais Injinia Hersi Said, kuondoka madarakani kwani uwapo wao haukufuata katiba ya klabu hiyo.
Inaelezwa kuwa uamuzi huu wa mahakama umekuja baada ya kundi la wazee wachache waliowahi kuwa wazee wa klabu hiyo kipindi cha nyuma kupeleka mashtaka mahakamani likidai uwapo wao hakufuata katiba.
“Novemba 6, mwaka 2022, watu wawili waljiita wanachama wa Yanga walifungua kesi katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, ambao ni Juma Ally (Magoma) aliyekuwa mlalamikaji namba moja na Geofrey Mwaipopo ambaye ni mlalamikaji namba mbili na wa tatu ni Jabir Katundu.
Walifungua dhidi ya Baraza la Wadhamini kama mlalamikiwa namba moja, mama Fatma Karume, Abeid Mohamed Abeid, ambaye ni mlalamikiwa namba tatu,” alisema wakili huyo.
Alisema walichokuwa wakihitaji ni kuondoka kwa viongozi waliopo, na mali za klabu na timu wakabidhiwe wao.
“Wanasema rais wa Klabu, Injinia Hersi, Makamu wake, Arafat Haji, Kamati ya Utendaji na watendaji wote walioajiriwa kwa kigezo cha unachama, wote uwanachama wao ni batili, hivyo hawafai kuiongoza klabu, hivyo walikuwa wanaiomba mahakama ituondoe wote.
Pia kazi zote ambazo zimefanywa na viongozi hao, zitambuliwe kama ni batili, hivyo waletewe ripoti ya mapato na matumizi kwa kipindi chote na klabu ikabidhiwe kwao,” alisema.
Hata hivyo, alisema walichogundua ni kwamba mmoja wa waliodai kuwa ni mjumbe wa Baraza la Wadhamini yupo upande wa walalamikaji.
“Tulichogundua ni kwamba iliendeshwa kwa upande mmoja, hao watu kugawana majukumu upande wa mlalamikaji na mlalamikiwa, kwa maana Juma na Mwaipopo walikaa upande wa mlalamikaji na Abeid alikaa upande wa mlalamikiwa, huku akiwawakilisha wadhamini.
“Katika shauri, Abeid, aliwasilisha utetezi wa mama Fatma uliosainiwa naye, pamoja Katundu, mlalamikiwa namba tatu, akidai wote wamemteua kuwawakilisha kwenye mwenendo wa kesi hiyo, na utetezi wa wote hao ulifanywa na yeye, hivyo alikuwa akikubali kila kitu kilichokuwa kikisemwa au kuombwa mahakamani, hivyo kusababisha hukumu ya Agosti 22, 2023 kuwapa ushindi walalamikaji kwa sababu haikuwa inapingwa,” alisema.
Alisema baada ya hukumu hiyo, Mei 24, mwaka huu, walipeleka maombi ya kukazia hukumu mbele ya Hakimu Mkazi, Kisutu, ikiwamo kulitoa na kulifuta baraza la wadhamini wa Yanga na kuutoa uongozi wote, kutaka wakabidhiwe timu na mali zote za klabu ili waendeshe wao, Juni 10 klabu lilipata taarifa hiyo, hivyo uongozi ulituma jopo la mawakili akiwamo yeye kufuatilia suala hilo kwa undani.
Alisema kufuatia hayo, jopo la wanasheria limetuma maombi kuomba waongezewe muda wa kufanya mapitio ya kesi na wanaamini wataitwa kusikilizwa kwa kuwa hawakushirikishwa.
“Klabu imetuma maombi ya kupitia upya kesi hiyo kwa sababu hatukushirikishwa na walalamikaji hawakuwa na uhalali wowote, vile vile walifanya kosa la jinai kufoji sahihi za viongozi wakubwa wa klabu tunaamini mahakama itatutendea haki na inaonekana kuna watu wanaowatumia kuleta uchochezi. Tumeanza uchunguzi na ikibainika, wahusika wote watapelekwa kwenye mkutano mkuu, pili tukishaongezewa muda, klabu itaomba kufanya marejeo kwa sababu walalamikaji wote hawakuwa na uhalali.
“Tatu ni maombi ya kuzuia utekelezaji wa hii hukumu ambayo walalamikaji waliiomba kuwasaidia kuuondoa uongozi wa Yanga na kukabidhiwa timu. Na nne, tumewasiliana na Mama Fatma na Katundu ili kushirikiana na uongozi wa Yanga kufungua kesi ya jinai kwa wote walioghushi saini zao kinyume cha matakwa yao,” alisema.