Bodi ya Ligi kukusanya maoni Udhamini wa Timu zaidi ya moja
Bodi ya Ligi imesema kuwa inakaribisha maoni ya wadau wote ambao wanaona hakuna haja ya mtu, kampuni au taasisi kudhamini zaidi ya timu moja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ili iundwe kanuni rasmi
Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Almasi Kasongo, amesema kuwa, kwa siku za karibuni kumeibuka hoja na mjadala kwa wadau wa soka ambao wanadhani kuna haja ya kuzuia mdhamini mmoja kudhamini zaidi ya timu moja, na kwa kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi wanaendesha soka kwa uwazi na usikivu, hawajafunga milango badala yake wanakaribisha maoni
Hata hivyo, Kasongo, amesema maoni hayo yatatolewa kwaajili ya kanuni ya msimu ujao, kwani msimu huu tayari wameshafunga na hakukuwa na mdau yoyote aliyelalamikia suala hilo.
“Hizi siku mbili tatu umekuwa mjadala mkubwa, lakini kwa wakati huu tuliokuwa nao hakuna kanuni inayozuia mdhamini mmoja kudhamini zaidi ya timu moja. Udhamini ni jambo la kikanuni, madhumuni ya kanuni kwa asilimia 90 yameelekezwa kwenye klabu husika, timu, wachezaji, waamuzi, viongozi, mbali na mijadala iliyoibuka, hakuna klabu yoyote au mdau kuelekea msimu huu aliyelalamikia suala hilo,” alisema Ofisa Mtendaji huyo
Hata hivyo, alisema kanuni siyo msahafu, hivyo kama wadau wataona kuna haja ya kuja na kanuni hizo, milango iko wazi
“Lakini mimi siku zote nimekuwa nikiamini kuwa kanuni siyo msahafu, zinajadilika, zinabadilishika kwa hiyo pale ambapo wadau wataona kuna haja ya kufanya mabadiliko ya kanuni kama ambavyo siku zote tumekuwa tukifanya basi milango ipo wazi,” alisema Kasongo
Alisema wao kama viongozi wa soka, wanataka kuongoza vile ambavyo wadau wa soka wataona inafaa na kuthamini michango yao.
Soma na hizi pia:
Tags: Bodi ya Ligi kukusanya maoni Udhamini wa Timu zaidi ya moja